BUSTANI YA HABARI

HABARI ZAKITAIFA

  RONALDO ABEBA TUZO TATU HISPNIA,MESSI AAMBULIA PATUPU

  Cristiano Ronaldo amekomba zawadi tatu 'hat trick' za tuzo ya wachezaji bora Ligi ya Hispania maarufu kama La Liga.

  Huku mpinzani wake Lionel Messi akiambulia patupu, tuzo tatu alizobeba Ronaldo ni pamoja na Mchezaji Bora, Mfungaji Bora na Mshambuliaji Bora wa La Liga.

  Ilikuwa furaha kubwa kwa Ronaldo ambaye aliongozana na mpenzi wake Iryna Shayk, mwanamitindo kutoka Urusi.
  Pamoja na Ronaldo kubeba tuzo hizo, timu yake ya Real Madrid imetawala zaidi kuliko klabu nyingine ya Hispania.
  Zawadi ya kiungo bora imekwenda kwa Luka Modric  huku Sergio Ramos akichukua tuzo ya beki bora.
  Kipa mpya wa Real Madrid, Keylor Navas amechukua tuzo ya mlinda mlango bora. Kabla ya kutua Madrid, Navas alikuwa akikipiga Levante.
  Barcelona pia imefanikiwa kupata tuzo tatu, Andrés Iniesta alitangazwa kuwa kiungo bora mshambuliaji, huku Ivan Rakitic na Rafinha wakitwaa tuzo mbili za Fair Play and Breakthrough.
  Kutokana na mafanikio makubwa msimu uliopita, Kocha wa Atlético, Diego Simeone alibeba tuzo ya Kocha Bora.

  Mshambuliaji nyota wa Sevilla, Carlos Bacca akachukua tuzo mchezaji Bora kutoka Amerika Kusini na Yacine Brahimi wa Granada akawa Mchezaji Bora kutoka Afrika.

  ACT TANZANIA WATOA TAARIFA KWA UMMA


  TAARIFA KWA UMMA

  Maazimio ya Mkutano wa Tatu wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Tanzania Uliofanyika Jumamosi Tarehe 25 Oktoba 2014 katika Hoteli ya Vina Jijini Dar es Salaam

  Kamati Kuu ya ACT-Tanzania ilifanya mkutano wake wa tatu siku ya Jumamosi tarehe 25 Oktoba 2014 katika Hoteli ya Vina Jijini Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilijadili na kutoa maazimio kuhusu hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu kama ifuatavyo:

  1Kamati Kuu imejadili hitimisho la mchakato wa Katiba Mpya katika ngazi ya Bunge Maalumu la Katiba. Kamati Kuu imeendelea kusikitishwa na kushindikana kupatikana kwa maridhiano baina ya makundi mbalimbali ya kisiasa nchini kuhusu mchakato na maudhui ya Katiba Mpya. Kamati Kuu imesikitishwa zaidi na uamuzi wa Chama cha Mapinduzi na serikali yake wa kuteka na kuburuza mchakato wa katiba kwa kuegemea matakwa ya sheria bila kujali uhalali mpana wa kisiasa na kijamii nchini.
  2.Kamati Kuu imezingatia kuwa mchakato wa katiba mpya umeitimishwa katika Bunge Maalumu la Katiba katika mtindo ambao umeacha mgawanyika na mpasuko mkubwa wa kisiasa na kijamii nchini badala ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa, ambalo ndilo lengo la msingi la mchakato wenyewe.
  3.Kutokana maelezo ya hapo juu (1 & 2), bila kujali uzuri au ubaya wa maudhui yaliyomo katika Katiba Inayopendekezwa, Chama cha ACT-Tanzania kitawashawishi wananchi kuikataa katiba inayopendekezwa kwa kupiga KURA YA HAPANA katika kura ya maoni.
  4.Kamati Kuu imesikitishwa na kuendelea kusuasua kwa kutolewa Ripoti kuhusu uchunguzi wa wizi wa fedha za umma uliofanyika kupitia akaunti ya Escrow iliyotokana na mgogoro baina ya TANESCO na IPTL. Kusuasua kutolewa kwa Ripoti ya Uchunguzu kumesababisha kukwamisha bajeti ya serikali kwa kuwa wafadhili wamesimamisha misaada muhimu kwa bajeti ya mwaka huu. Kamati Kuu inamtaka CAG atoe Ripoti yake kwa Kamati ya PAC kwa ratiba iliyopangwa. Aidha Kamati Kuu inawaunga mkono wabunge wote walio mbele katika kupigania sheria kuchukua mkondo wake katika sakata hili. Kwa kipekee, Kamati Kuu imempongeza Mhe David Kafulila kwa ujasiri wake katika kuhakikisha kwamba sheria inachukua mkondo wake kwa wote waliohusika na wizi wa fedha za umma kupitia kivuli cha akaunti ya Escrow. Tunawahimiza wabunge wazalendo wamuunge mkono mbunge mwenzao Mhe Kafulila katika kuhakikisha kwamba uwajibikaji unapatikana katika kashfa hii kubwa kabisa kuikumba nchi yetu.
  5.Kamati Kuu imepokea taarifa ya kuhusu ufadhili wa wanafunzi wa elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo. Kamati Kuu imesikitishwa na taarifa kwamba zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini hawatapata mikopo. Kamati Kuu haikubaliani na hali hii na imewahimiza wanafunzi, vijana na wadau wa elimu nchini kuungana na chama cha ACT-Tanzania katika kuishinikiza serikali kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa wanapatiwa mikopo ili wawezi kujipatia elimu ya juu ambayo inahitajika sana kwa mustakabali wan chi yetu.
  6.Uzinduzi rasmi wa chama utafanyika katika jiji la Dar es salaam mnamo tarehe 05 Desemba mwaka huu. Kwa mujibu wa katiba ya ACT TANZANIA kuna mkutano mkuu wa kidemokrasia (NATIONAL DEMOCRATIC CONGRESS). Mkutano wa kwanza wa namna hiyo utafanyika Desemba 5. Tunatoa wito kwa wanachama wote Tanzania kuanza maandalizi ya kushiriki mkutano huu.
  7.Kutakuwa na mapokezi makubwa na mkutano mkubwa wa kwanza wa hadhara katika jiji la mwanza siku inayofuata tarehe 06 dec 2014. Wito kwa wakazi wa jiji kufanya maandalizi makubwa kukipokea chama mbadala
  8.Mwisho Kamati kuu imeazimia kushiriki kwa nguvu zote uchaguzi serikali za mitaa na imeridhika na maandalizi ya kupata wagombea katika ngazi ya mitaa,vijiji na vitongoji.


  Samson Mwigamba
  Katibu Mkuu
  Jumatatu, 27 Oktoba 2014

  SOMA MAKALA MAALUMU"MAFANIKIO NA UTATA WA MEMBE KIDIPLOMASIA"

  "MAFANIKIO NA UTATA WA MEMBE KIDIPLOMASIA
  Kitila Mkumbo
  KATIKA makala iliyopita nilianza kumjadili Benard Membe anayetajwa kuwa kati ya wagombea urais wenye nafasi kubwa ya kupitishwa kupeperusha bendera ya chama chake cha CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
  Katika makala haya ninajadili wasifu wa Membe katika maeneo ya kazi, uadilifu na diplomasia.
  Kikazi, tunaweza kusema Membe ni mtu aliyekulia katika ushoroba wa madaraka (power corridors). Mara baada ya kumaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, Membe aliajiriwa kufanya kazi katika ofisi ‘nyeti’ ya Rais. Na hata baada ya kuhitimu masomo yake ya shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alirudi kuendelea na kazi yake ya ukachero na hivyo kushindwa kuchukua kazi aliyokuwa amepewa ya uhadhiri msaidizi katika Chuo hicho.
  Membe alipanda ngazi kadhaa na hata kuwa msaidizi wa waliopata kuwa wakurugenzi wakuu wa Idara nyeti ya Usalama wa Taifa, Dk. Hans Kitine na Apson Mwang’onda.
  Baada ya kumaliza masomo ya Shahada ya Uzamiri katika Chuo Kikuu cha John Hopkins nchini Marekani, Membe hakurudi tena kufanya kazi Ikulu bali alipelekwa ubalozi wa Tanzania nchini Canada kama Mwambata wa Ubalozi (Minister Plenipotentiary), akichukua nafasi ya Dk. Augustine Mahiga akiyekuwa amehamishiwa Umoja wa Mataifa.
  Alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2000 alipoamua kugombea ubunge, akashinda na kuwa Mbunge wa pili wa Jimbo jipya la Mtama, akimrithi Masoud Ally Chitende.
  Katika kampeni za urais za mwaka 2005 ndani na nje ya CCM Membe alifanya kazi kwa karibu na akina Edward Lowassa na Apson katika kuhakikisha kwamba Jakaya Kikwete anapitishwa kuwa mgombea na hatimaye kushinda katika uchaguzi wa urais.
  Inafurahisha na hata kushangaza kwamba hawa leo ni mahasimu wakubwa kisiasa wote wakiwania nafasi ya kumrithi Rais Kikwete.
  Tutarajie ushindani mkali hasa ndani ya CCM kati yao, ambao wanaonekana kuwa na nguvu, fursa, vikwazo na udhaifu katika maeneo tofautitofauti.
  Baada ya Rais Kikwete kushinda uchaguzi wa mwaka 2005 alimteua Membe kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini nafasi aliyoshikilia kati ya Oktoba 2006 na Januari 2007, na baadaye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kati ya Januari 2006 na Oktoba 2006. Baada ya kuteuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete alimteua Membe kuchukua nafasi yake.
  Katika mawaziri 14 wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimataifa, Membe ndiye waziri wa pili kwa kushikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu zaidi, akizidiwa tu na Rais Kikwete aliyedumu katika nafasi hiyo katika kipindi chote cha urais wa Mkapa.
  Taswira ya Membe katika uadilifu
  Bernard Membe ni kati ya viongozi wachache katika serikali ya CCM wanaojitutumua kwamba ni waadilifu.
  Msingi wa uadifu wa Membe unajengwa katika maeneo mawili makubwa. Eneo la kwanza ni kazi aliyoifanya kuokoa fedha za umma kwa kutumia nafasi aliyoishika katika ubalozi wa Canada.
  Mapema katika Bunge la mwaka 2001/2002, paliibuka kashfa kubwa ikimhusisha aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora Dk. Hans Kitine. Katika kashfa hiyo ilidaiwa kwamba Dk. Kitine alikuwa ametumia fedha za serikali kwa kumtibu mke wake, Saada Mkwawa Kitine, nje ya nchi kwa kiwango cha dola za kimarekani 63,000.
  Hata hivyo, uchunguzi wa Serikali haukuonyesha ushahidi wowote kwamba mke wa Dk. Kitine alitibiwa nje ya nchi wala kuumwa. Kashfa hii ikasababisha Dk. Kitine kujiuzulu nafasi yake na mke wake kuamriwa kulipa fedha zote alizokuwa amechukua kwa matibabu hewa.
  Hata hivyo, mwezi Julai 2002, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mbunge Richard Ndasa aliyekuwa anakaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, iliandika barua Wizara ya Afya ikiiagiza wizara hiyo kumrudishia mke wa Kitine pesa ambazo alikuwa ameshalipa kiasi cha dola 15,000. Kamati hiyo ilidai kugundua kwamba Mama Kitine alikuwa kweli anaumwa na alitibiwa nje ya nchi kwa kufuata utaratibu.
  Haraka haraka Dk. Kitine akaitisha mkutano na waandishi wa habari na kujigamba kwamba yeye ni mwadilifu na kilichotokea ilikuwa ni majungu tu na hivyo Bunge limemsafisha.
  Ni katika hatua hii ambapo Bernard Membe alisimama Bungeni kueleza kwamba alikuwa na ushahidi bayana kuhusu ufisadi uliofanywa na Dk. Kitine kwa jina la matibabu ya mke wake.
  Alipopewa nafasi, Membe akamwaga nyaraka muhimu zilikuwa zinaonyesha jinsi fedha zilivyotumwa kwenye akaunti binafsi ya mama Kitine badala ya kutumwa
  katika akaunti ya ubalozi. Membe akiwa ubalozini Canada ndiye aliyepewa jukumu la kuchunguza uhalali wa matibu na malipo kwa ajili ya mama Kitine.
  Katika hospitali zote zilizodaiwa kumtibu mama Kitine hawakupata ushahidi wowote kwamba aliwahi hata kufika huko, achilia mbali kutibiwa.
  Kufuatia kuthibitika kwa kashfa ya Dk. Kitine, ilionekana wazi kwamba Kamati ya Bunge ilikuwa imetumika kujaribu kumsafisha Dk. Kitine na familia yake kwa njia za giza. Kwa sababu hii wajumbe watatu wa Kamati hii walifungiwa miezi miwili kihudhuria vikao vya Bunge. Wajumbe hawa walikuwa ni Richard Ndasa, Dk. Amani Kaborou na Dk. Hans Kitine mwenyewe.
  Eneo la pili ni maelezo kwamba Membe ni mjumbe pekee wa Halmashauri Kuu aliyeshinda uchaguzi ndani ya chama chake mwaka 2012 kupitia kundi linaloitwa la kifo bila kuhonga wajumbe wa Mkutano Mkuu.
  Katika uchaguzi huu Membe alichaguliwa kwa kura 1451, nyuma ya Wasira, Mwigulu Nchemba na Makamba, huku akipigwa vita kali na mahasimu wake waliopo katika kundi la Lowassa.
  Mahasimu wake Membe wanakataa kwamba hakutumia pesa katika kushinda nafasi ya NEC. Hata hivyo, wanakiri kwamba walifanya kampeni dhidi yake ili ashindwe!
  Mafanikio na Utata wa Membe kidiplomasia
  Mafanikio na utata wa Membe kidiplomasia unaonekana katika maeneo mengi. Kwanza ni katika misimamo mbalimbali ambayo amekuwa akiitoa kwa niaba ya Tanzania.
  Kwa mfano, amekuwa na msimamo wa wazi wa kumtetea Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe wakati ambapo mataifa ya Magharibi yakiwa yamemtenga na kutomtambua.
  Hii inaweza kumtambulisha kama mzalendo wa Afrika (Pan Africanist). Aidha, Membe alisita kwa kipindi kirefu kuutambua utawala mpya wa Libya baada ya kupinduliwa kwa Rais Gadafi. Hata hivyo, baadhi ya watu walidhani kwamba Tanzania ingekuwa nchi ya kwanza kuutenga utawala wa Gadafi ukizingatia kwamba huyu ni mtu aliyetusaliti katika vita yetu na Idd Amin kwa kusaidia majeshi ya Uganda.
  Pengine alama kubwa zaidi za mafanikio ambazo Membe anaweza kutembea nazo katika anga za kidiplomasia ni mbili. Mosi, ni kuchaguliwa kwake hivi karibuni kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CMAG) mwezi Novemba 2013 huko Sri Lanka. Hii ni Kamati yenye nguvu sana katika Jumuiya ya Madola yenye majukumu mengi, ikiwamo kufukuza nchi uanachama wa Jumuiya hiyo. Kabla ya Membe, mara nyingi wenyeviti wa Kamati hii walitoka katika nchi zilizoendelea.
  Alama ya pili ni jinsi alivyofanikisha ujio wa Marais wawili wakubwa duniani: Xi Jinping wa China na Barack Obama wa Marekani. Aidha, aina ya mapokezi waliyoandaliwa viongozi hawa yanaelezwa kuwa ya kiwango cha juu kiasi cha kusababisha kiwewe kwa nchi majirani.
  Hata hivyo, kuna maeneo kadhaa yanayoonyesha utata kuhusu weledi wa Membe katika diplomasia. Kwa mfano, Membe aliitangazia dunia kupitia Bunge letu Mei 27, 2014 kwamba waasi wa kikundi cha M23 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa walikuwa ni raia wa Rwanda na walikuwa wakifadhiliwa na Serikali ya Rwanda.
  Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kuituhumu waziwazi Serikali ya Rwanda katika kufadhili kikundi hicho cha waasi katika kipindi ambacho uhusiano wa nchi mbili hizi ulikuwa unalegalega.
  Kabla moto haujapoa, Mkumbwa Ally akikaimu nafasi ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliwaambia waandishi wa habari Julai 12 2013 kwamba “….Rwanda iachane na ndoto zake za kuivamia Tanzania; vinginevyo ...Kagame tutamtandika kama mtoto mdogo”.
  Katika hali ya kawaida, na kwa kuzingatia nafasi ya Tanzania katika Afrika, haikutarajiwa kwamba Membe na Wizara yake wangemkabili Rais Paul Kagame kwa diplomasia ya kibabe.
  Eneo jingine ambalo ni tata kuhusu diplomasia ya Membe ni sera ya diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Serikali ya Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.
  Kupitia demokrasia hii, balozi zetu zimekuwa na kazi kubwa ya kuvutia wawekazaji na kwa kweli zimefanikiwa sana kufanya kazi hii.
  Hata hivyo, ni kipindi hiki pia ambacho nchi yetu imepokea wawekezaji wa ajabu ambao wamegeuka kuwa waporaji wa raslimali zetu na wengine kuingiza nchi yetu katika giza nene la ufisadi.
  Ni katika kipindi hiki pia ambacho nchi yetu imegeuka kuwa ombaomba, na hatimaye, kupoteza kabisa msamiati wa ‘Kujitegemea’ katika falsafa za maendeleo Tanzania.
  Aidha, kwa kiasi kikubwa, Tanzania imepoteza nafasi iliyokuwa nayo katika Bara la Afrika. Kwa mfano, wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kwanza Tanzania ndiyo ilikuwa kiongozi lakini sasa tumekuwa ndio kikwazo cha Jumuiya hii na tumekuwa tukibembelezwa na kuburuzwa.
  Tumewekeza zaidi kukubalika katika mataifa ya Wazungu na kusahau kabisa Afrika. Haishangazi basi kuona kwamba leo hii Rais wetu amefanya ziara nyingi zaidi Marekani na Ulaya kuliko alizofanya Afrika.
  Inashangaza, kwa mfano, hadi niandikapo makala hii Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya hajawahi kufanya ziara ya kikazi rasmi Dar es Salaam zaidi ya mwaka mmoja tangu achaguliwe.
  Eneo la tatu ni msimamo wa Membe kuhusu uraia pacha. Waziri Membe na Rais Kikwete wamekuwa na msimamo wa waziwazi wa kuunga mkono uraia pacha kinyume cha msimamo wa Julius Nyerere wa mwaka 1962 aliyepinga uraia huo.
  Kwa baadhi ya watu uraia pacha ni jambo la maana na wanamuona Membe kama mtu anayekwenda na wakati na msimamo huu unakwenda sambasamba na diplomasia ya uchumi. Kwa watu wengine, hata hivyo, kuunga mkono uraia pacha ni kukosa uzalendo.
  Hitimisho
  Bila shaka kuna mambo mengi yanayombeba Membe kama mgombea urais kihaiba na kikazi. Kwanza ana msimamo. Bila kujali uhasi na uchanya wa misimamo yake, kuwa na msimamo ni jambo la msingi kwa kiongozi.
  Msimamo wake mkali dhidi ya mambo kadhaa kimataifa na kukulia kwake katika kazi ya ukachero yamewafanya baadhi ya watu kufananisha haiba ya Membe na ile ya Rais Vladimir Putin wa Russia aliyekulia Kremlin.
  Hata hivyo, ili avae haiba ya Putin sawasawa, itamlazimu kuuvaa ukali kidogo kwa kuwa baadhi ya watu waliopo naye karibu wanamueleza kuwa ni mtu mpole na mwepesi wa huruma. Hii inaweza ikawa kasoro kwa baadhi ya watu wanaoamini kwamba Tanzania ilipofika haihitaji Rais mpole wala mwenye huruma.
  Pili, Membe anajitambulisha kwa taswira ya uadilifu na kwa kweli ni vigumu kumhusisha na kashfa yeyote iliyotokea hapa nchini.
  Kwa mfano, Membe hatajwi popote katika Ripoti ya Dk. Harrison Mwakyembe iliyochunguza kashfa ya Richmond licha ya ukweli kwamba yeye alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Hata hivyo, Membe ana kazi ya ziada katika kujenga imani kwamba ana taswira tofauti na chama chake katika eneo la uadilifu.
  Tatu, Membe anajivunia rekodi ya kuipaisha Tanzania katika anga za kimataifa,kidiplomasia. Hata hivyo, ana maswali ya kujibu kutokana na taswira ya Tanzania kufifia katika diplomasia ya Afrika na hasa kusuasua kwa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
  Ni wazi kuwa Membe ana alama kadhaa chanya za kiuongozi zinazojionyesha katika utendaji wake sehemu mbalimbali alizofanya kazi. Hata hivyo, anayo kazi katika kuzinadi alama hizi katika jamii ili zimjengee taswira ya uchapa kazi, ambayo ni moja ya sifa muhimu za rais wa awamu ya tano.
  Ninamtakia kila la heri Bernard Kamillius Membe katika mbio zake za kuwania uongozi wa juu katika nchi yetu"
  (Prof. Kitila Mkumbo, Raia Mwema, Toleo la 375, Octoba 15, 2014)
  www.raiamwema.co.tz/mafanikio-na-utata-wa-membe-kidiplomasia

  WACHEZAJI WATATU SIMBA KIFUNGONI


  Wakati Simba leo inaingia kambini Makambako mkoani Iringa kuwawinda Mtibwa Sugar, wachezaji watatu wa kikosi cha kwanza Shabani Kisiga, Amri Kiemba na Haruna Chanongo wamesimamishwa kwa muda.
  Kwa upande wa kocha mkuu Patrick Phiri, akizungumzia matokeo ya mechi ya juzi ambayo Chanongo na Kiemba waliingia wakitokea benchi huku Kisiga akiishia ‘kusugua mkeka’, alisema lawama kutokana na matokeo mabovu katika mechi dhidi ya Prisons inapaswa kuelekezwa kwa timu nzima.
  Simba iliyokuwa imeahidi kupata ushindi wa kwanza msimu huu katika mechi yake ya raundi ya tano, ilijikuta ikiambulia sare ya tano mfululizo baada ya kutoka 1-1 na wenyeji Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini hapa juzi.
  Phiri aliwaomba wanachama, wapenzi na mashabiki wa Simba kutomlaumu mchezaji au mtu yeyote ndani ya klabu hiyo badala yale waelekeza lawama kwa timu nzima.
  “Tumeamua kukaa Mbeya kwa siku moja zaidi ili leo (jana) jioni tupate fursa ya kuwaangalia Mtibwa Sugar wakicheza dhidi ya Mbeya City hapa. Kesho (leo) asubuhi tutaanza safari ya kurejea lakini tutaweka kambi Makambako kujiandaa kwa mechi yetu inayofuata dhidi ya Mtibwa,” Phiri alisema.
  “Jana (juzi) tulionekana kushinda mechi lakini tukarudia kosa lililotugharimu katika mechi zetu tatu za mwanzo. Ninaomba asilaumiwe mtu yeyote kutokana na matokeo hayo. Kama timu, sote tunapaswa kulaumiwa kutokana na matokeo haya.
  “Timu imekuwa ikikosa umakini wa mchezo, hasa kipindi cha pili na kujikuta tunaruhusu mabao mepesi. Tutaendelea kufanyia kazi tatizo hili ili tuwe na kikosi cha ushindani,” aliongeza.
  Aidha, kocha huyo aliyerejea kwa mara ya tatu nchini kuinoa Simba baada ya kuifundisha pia 2005 na 2010 huku akiipa ubingwa bila kupoteza hata mechi moja, alisema timu yake bado ina nafasi ya kuwania ubingwa wa VPL.
  “Bado tuna nafasi ya kutwaa ubingwa msimu huu,” alisema. “Kwa sababu tuna pointi tano, walioko juu ya msimamo wa ligi wana pointi 10 tu (kabla ya mechi ya jana baina ya Mbeya City na Mtibwa Sugar).”
  SOURCE:KANDANDA

  SAMUEL ETO'O AENDELEA KUTAMBA AKIWA NA EVERTON


  Mshambulia ji wa klabu ya Everton Samuel Eto'o juzi alionyesha kuwa bado yuko vizuri baada ya kupachika mabao mawili na kuipa timu yake ya Everton ushindi dhidi ya Burnley.
  Burnley walikubali kichapo cha mabao 3-1 wakiwa katika uwanja wao wa nyumani, Samuel Eto'o alianza kufungua mlango wa Burnley dakika ya 4 tu ya mchezo kabla ya Danny Ings wa Burnley kusawazisha dakika ya 20 .Romelu Lukaku akaandi bao 2 katika dakika ya 29 ya mchezo na kwenda mapumziko wakiwa wako mbele kwa mabao 2-1.
  Kipindi cha pili kiliaanza huku Everton wakionekana kuwa vizuri sana sehemu zote, Samuel Eto'o kwa mara nyingine dakika ya 86 akapachika bao la 3 kwa Everton.

  DONDOO ZA AFYA:UFAHAMU UGONJWA WA EBOLA KWA KINA

  Ugonjwa wa Ebola unasababishwa na Virusi na ni ugonjwa hatari unaoambukiza haraka binadamu na wanyama mwitu (hayawani) kama kima, sokwe, popo, ndege, mijusi, amfibia, na kadhalika. Ugonjwa huu unaosababishwa na virusi aina ya Ebola Virus ni wa mlipuko.
  Japokuwa hakuna mazingira maalum ambamo virusi vya Ebola vinapatikana, lakini wataalamu wanasema virusi hivyo vinapatikana kwa mnyama ambaye anapatikana zaidi barani Afrika.
  Mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola umetokea katika nchi nyingi na bado unaendelea kupukutisha maisha ya watu wengi hasa barani Afrika. Matukio ambayo yamethibitishwa kuwepo kwa ugonjwa huo ni katika nchi za Liberia, Sierra Leone, Guinea, Ghana, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Gabon, Sudan, Ivory Coast, Uganda na kadhalika.

   
  Ugonjwa wa Ebola daima unasambaa ndani ya maeneo ya utoaji wa huduma za afya.Hata hivyo, matukio mengine yamekuwa yakitokea nje ya maeneo hayo na hayafahamiki.
  Jinsi ugonjwa huo unavyosambaa:
  Namna ugonjwa huo ulivyojulikana kwa mara ya kwanza hakuna anayefahamu kwa hakika. Hata hivyo, ugonjwa wa Ebola unaweza kusambazwa kwa njia zifuatazo:
  1. Kugusana moja kwa moja na mtu ama mnyama mwenye ugonjwa huo;

  2. Kugusana moja kwa moja na damu ama majimaji (mate au mafua) ya mtu mwenye ugonjwa huo katika familia;

  3. Kugusa vifaa vya tiba vilivyo na virusi vya ugonjwa huo kama sindano;

  4. Kutumia vifaa visivyochemshwa katika hospitali kama sinano;

  5. Kula ama kushika vinyesi vya wanyama wenye ugonjwa huo;
  6. Kuvuta hewa yenye virusi vya ugonjwa huo katika mazingira ya hospitali;
  7. Kutumia nyama ya wanyama walioathirika kama kitoweo;
  8. Kutozingatia tahadhari za kitaalam.

  Dalili za Ebola:
  Mtu au mnyama mpaka aonyeshe dalili za ugonjwa wa Ebola huchukua kati ya siku 2 hadi 21. Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na:
  1. Homa kali
  2. Kuumwa kichwa

  3. Kuharisha

  4. Kutapika

  5. Maumivu ya kifua

  6. Maumivu ya tumbo
  7. Mafua
  8. Kikohozi
  9. Maumivu ya misuli na viungo, hasa kwenye viungio
  10. Kuvimba koo
  11. Mwili kuwa dhaifu
  12. Mfadhaiko
  13. Kuchanganyikiwa
  14. Macho kuwa mekundu
  15. Kuvuja damu kwa ndani na nje

  Nani aliye katika hatari?
  1. Watu wanaofuga wanyama mwitu ama wanaoishi katika maeneo yenye wanyama mwitu;

  2. Watu wanaotegemea wanyama mwitu kama popo kama chakula chao;

  3. Watumishi wa vyumba ya kuhifadhia maiti;

  4. Watumishi wa afya wanaowahudumia wagonjwa wa Ebola;

  5. Watumishi wa afya katika hospitali ambazo hazina mazingira bora na safi;
  6. Wanafamilia wa wagonjwa wa Ebola;
  7. Watu wanaohudhuria hospitali ambazo hazina mazingira safi na salama;

  Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola:
  1. Epuka kugusa damu/majimaji ya wanyama ama binadamu walio na ugonjwa wa Ebola au hata maiti za watu waliokufa kwa ugonjwa huo kwa kuzingatia haya:
  a) Tunza mazingira safi na salama ya hospitali;

  b) Watelekeze wagonjwa wa Ebola;

  c) Fukia miili ya waliokufa kwa Ebola kwa usalama;

  d) Epuka mazishi ya kienyeji kama kuosha maiti za watu waliokufa kwa Ebola;

  2. Watumishi wa afya na wanaowatazama wagonjwa wa Ebola wanatakiwa:
  a) Kuvaa kwa usahihi vifaa vya kujikinga na nyuso, mikono na macho,

  b) Na majoho maalum daima;

  c) Kutumia sindano mara moja na kuziteketeza ama kuzifukia;

  d) Epuka kutumia zaidi ya mara moja sindano au kutotumia sindano ambazo hazijachemshwa vyema;

  e) Epuka kuosha maiti za watu waliokufa kwa Ebola;
  CHANZO : BROTHER DANY BLOG

  MBWA WAKUTWA WAKILA MABAKI YA MWILI WA BINAADAMU

   Mabaki ya mwili yaliyokutwa katika eneo la kijiji cha Lupapila wilaya ya songea mkoaniRuvuma yakikusanywa na wataaramu kutoka hospital ya mkoa wa Ruvuma.
  Fuvu la kichwa likiwa linazolewa 
  -------------
  Na Amon Mtega wa Demasho.com Songea

   MIFUPA ya masalia ya binadamu  wa jinsia ya kiume  ambaye hakuweza

  kufahamika  jina na kukadiliwa kuwa na miaka (30) yamegundulika na  Zaujia Pilly (70) mkazi wa kijiji cha Lupapila wilaya ya songea mkoani

  Ruvuma  wakati akienda kuchimba dawa za kienyeji baada ya kuwaona mbwa
  wakishambulia sehemu za mabaki hayo.  Akiongea na MTANDAO HUU ofisini kwake jana Kamanda wa polisi mkoa wa
  Ruvuma Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo limetokea oktoba 26
  mwaka huu majira ya saa 9:45  alasiri  huko katika kijiji cha Lupapila
  mtaa wa Mahinya kata ya Subira nje kidogo ya manispaa ya Songea.  Alisema kuwa  inadaiwa siku hiyo ya tukio kwenye msitu wa uwanja wa
  ndege ilikutwa mifupa ya binadamu  wa jinsia ya kiume  ikiwemo fuvu la
   Kichwa, Mbavu, Mikono na Miguu wakati sehemu ya kiuno na mapaja ikiwa
  imeharibika vibaya.  Alifafanua kuwa mabaki ya mwili huo yaligunduliwa na Zaujia Pilly
  wakati akienda kuchimba dawa za kienyeji kwenye msitu huo ghafla
  aliwaona Mbwa wakifukuzana kugombania mabaki ya mwili wa binadamu.  Alieleza zaidi kuwa  Zaujia baada ya kugundua tukio hilo alitoa
  taarifa katika uongozi wa serikali ya Mtaa na kisha taarifa
  zilipelekwa katika kituo kikuu cha polisi cha songea mjini ambako
  baadaye polisi walifika eneo la tukio wakiwa wameongozana na Daktari
  kutoka hospitgali ya Mkoa wa Ruvuma ambaye aliyafanyia uchunguzi
  mabaki ya mwili huo na kubaini kuwa  marehemu alikuwa amepigwa na kitu
  kizito kichwani kwenye eneo la kisogo kilichopelekea kifo chake.  Kamanda Msikhela alisema kuwa  kufuatia tukio hilo hakuna mtu yeyote
  anayehusishwa na jeshi la polisi mkoani Ruvuma linaendelea kufanya
  uchunguzi wa kina juu ya kifo hicho.  CDT: Demasho.com 

DONDOO ZA AFYA